JERRY MURO AAAMKA, ATAKA SIMBA, YANGA WAUNGANE KUPAMBANA NA UONEVU WA TFF
Aliyekuwa
Mkurugenzi wa Habari wa Yanga, Jerry Muro amesema Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) limefanikiwa kuwagawanya Simba na Yanga na sasa
linawatawala linavyotaka bila kufuata kanuni.
Muro amesema TFF imekuwa ikifungia wadau hasa wale wanaojaribu kuueleza ukweli uongozi wa shirikisho hilo unapokuwa si sahihi.
“Hii nilisema tokea mwanzo, kwamba tushirikiane. Lakini Simba hawakunielewa na waliendelea kufurahia mimi kufungiwa kwangu.
“Sasa Yanga nao wanafurahia kufungiwa kwa Manara. Wamefanikiwa kutugawanya na wanaendelea kututawala wanavyotaka, hii si sahihi.
“Kitu kibaya zaidi TFF wanaendelea kuishi wanavyotana na wana uhakika wa kurejea tena ili waendelee kufanya wanavyotaka.
“Hii si sawa na maendeleo ya mpira wa Tanzania hayana uhakika tena, nawashauri ndugu zangu tuungane kuhakikisha kuna mabadiliko.
“Kuna
mambo ya ushindani na kuna mambo ya kushirikiana pamoja na kufanya
mambo kwa ajili ya mpira wa Tanzania. Tusiwape nafasi watu wanaotuvuruga
waendelee kututawala wanavyotaka,” alisema.
TFF imeendelea kuwafungia wanamichezo wote wanaoonyesha nia ya kuikosoa kwa nguvu hasa pale inapofikia kuendesha mambo kienyeji.
Malalamiko
yamezidi kuongezeka kadiri siku zinavyosonga mbele lakini TFF
wanaonekana kutosikiliza huku wakiendelea kuwaadhibu wadau mbalimbali
kwa matakwa yao binafsi.