UNICEF YATOA RIPOTI KUHUSU HALI YA NDOA ZA UTOTONI DUNIANI

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetoa ripoti
inayoeleza kupungua kwa kesi za mimba katika umri mdogo duniani kote.
Shirika hilo limeeleza kuwa takribanI ndoa za utotoni Milioni 25
zimezuiwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambapo kwa sasa mtoto
mmoja kati ya watano wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18 ukilinganisha
na mmoja kati ya wanne aliyekuwa anaolewa kipindi hicho.
Nchi za kusini mwa Bara la Asia pia zimepunguza ndoa za utotoni huku
Afrika ikiendelea pia kujitahidi kukabiliana na tatizo hilo ambapo kwa
nchi kama Ethiopia imepunguza tatizo hilo kwa theluthi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mzigo wa ndoa za utotoni unaendelea kuzilemea
nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako jitihada zaidi zinahitajika
ili kuondoa tatizo hilo kabisa.
UNICEF inasema kuwa mmoja kati ya watoto watatu wanapitia ndoa za
utotoni kwa kipindi hiki Afrika ukilinganisha na mmoja kati ya watoto
watano waliokuwa wakiolewa miaka kumi iliyopita.
Viongozi wa dunia wameapa kumaliza tatizo la ndoa za utotoni ifikapo
mwaka 2030 chini ya Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).